Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 4:1-11

Maombolezo 4:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Jinsi gani dhahabu yetu ilivyochujuka, dhahabu safi kabisa ilivyobadilika! Mawe ya thamani yametawanywa yamesambaa barabarani kote. Watoto wa Siyoni waliosifika sana, waliothaminiwa kama dhahabu safi, jinsi gani sasa wamekuwa kama vyombo vya udongo, kazi ya mikono ya mfinyanzi! Hata mbwamwitu huwa na hisia za mama na kuwanyonyesha watoto wao; lakini watu wangu wamekuwa wakatili, hufanya kama mbuni nyikani. Midomo ya watoto wachanga imekauka kwa kiu, watoto wanaomba chakula lakini hakuna anayewapa. Watu waliojilisha vyakula vinono sasa wanakufa njaa barabarani. Waliolelewa na kuvikwa kifalme sasa wanafukua kwa mikono kwenye majaa. Watu wangu wamepata adhabu kubwa kuliko watu wa mji wa Sodoma mji ambao uliteketezwa ghafla bila kuwa na muda wa kunyosha mkono. Vijana wa Siyoni walikuwa safi kuliko theluji, walikuwa weupe kuliko maziwa. Miili yao ilikuwa myekundu kama matumbawe, uzuri wa viwiliwili vyao kama johari ya rangi ya samawati. Sasa sura zao ni nyeusi kuliko makaa, wanapita barabarani bila kujulikana; ngozi yao imegandamana na mifupa yao imekauka, imekuwa kama kuni. Afadhali waliouawa kwa upanga kuliko waliokufa kwa njaa, ambao walikufa polepole kwa kukosa chakula. Kina mama ambao huwa na huruma kuu waliwapika watoto wao wenyewe, wakawafanya kuwa chakula chao wakati watu wangu walipoangamizwa. Mwenyezi-Mungu alionesha uzito wa ghadhabu yake, aliimimina hasira yake kali; aliwasha moto huko mjini Siyoni ambao uliteketeza misingi yake.

Maombolezo 4:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Jinsi dhahabu ilivyopoteza mngʼao wake, dhahabu iliyo safi haingʼai! Vito vya thamani vimetawanywa kwenye mwanzo wa kila barabara. Wana wa Sayuni wenye thamani, ambao mwanzo uzito wa thamani yao ulikuwa wa dhahabu, sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo, kazi ya mikono ya mfinyanzi! Hata mbweha hutoa matiti yao kunyonyesha watoto wao, lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma kama mbuni jangwani. Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga umegandamana na kaakaa la kinywa chake, watoto huomba mkate, lakini hakuna yeyote awapaye. Wale waliokula vyakula vya kifahari ni maskini barabarani. Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau sasa wanalalia majivu. Adhabu ya watu wangu ni kubwa kuliko ile ya Sodoma, ambayo ilipinduliwa ghafula bila kuwepo mkono wa msaada. Wakuu wao walikuwa wamengʼaa kuliko theluji na weupe kuliko maziwa, miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani, kuonekana kwao kama yakuti samawi. Lakini sasa ni weusi kuliko masizi; hawatambulikani barabarani. Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao, imekuwa mikavu kama fimbo. Wale waliouawa kwa upanga ni bora kuliko wale wanaokufa njaa; wanateseka kwa njaa, wanatokomea kwa kukosa chakula kutoka shambani. Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma wanapika watoto wao wenyewe, waliokuwa chakula chao watu wangu walipoangamizwa. BWANA ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake; ameimwaga hasira yake kali. Amewasha moto katika Sayuni ambao umeteketeza misingi yake.