Luka 16:19-31
Luka 16:19-31 Biblia Habari Njema (BHN)
“Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku. Na, mlangoni pa huyo tajiri kulikuwa na maskini mmoja jina lake Lazaro, ambaye alikuwa amejaa vidonda. Lazaro alitamani kupewa makombo yaliyoanguka kutoka mezani pa huyo tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kuramba vidonda vyake! “Basi, huyo maskini akafa, nao malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa. Huyo tajiri, akiwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye. Basi, akaita kwa sauti: ‘Babu Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.’ Lakini Abrahamu akamjibu: ‘Kumbuka mwanangu kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa. Licha ya hayo, kati yetu na nyinyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, na wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.’ Huyo aliyekuwa tajiri akasema: ‘Basi babu, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu, maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.’ Lakini Abrahamu akamwambia: ‘Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.’ Lakini yeye akasema: ‘Sivyo babu Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka kwa wafu na kuwaendea, watatubu.’ Naye Abrahamu akasema: ‘Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka kwa wafu.’”
Luka 16:19-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa walikuwa wakija na kumramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Abrahamu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Abrahamu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Abrahamu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, aupoze ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Abrahamu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo yako mema katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unateseka. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Abrahamu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Abrahamu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishika hata mtu akifufuka katika wafu.
Luka 16:19-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.
Luka 16:19-31 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake. “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. Kule Kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Ibrahimu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa kifuani mwake. Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’ “Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’ “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani mwa baba yangu, maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’ “Ibrahimu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Musa na Manabii, wawasikilize hao.’ “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Ibrahimu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’ “Ibrahimu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Musa na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”