Luka 17:20-37
Luka 17:20-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati mmoja, Mafarisayo walimwuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Naye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa namna itakayoweza kuonekana. Wala hakuna atakayeweza kusema, ‘Uko hapa’, au ‘Uko pale’. Kwa kweli ufalme wa Mungu uko kati yenu.” Halafu akawaambia wanafunzi wake, “Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona. Na watu watawaambieni: ‘Tazameni, yuko pale!’ Au ‘Tazameni, yupo hapa!’ Lakini nyinyi msitoke wala msiwafuate. Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku ile yake. Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki. Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu. Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote. Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga. Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na madini ya kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote. Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa. “Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke kwenda nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma. Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti. Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa. Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” [ Watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.] Hapo wakamwuliza, “Ni wapi Bwana?” Naye akawaambia, “Palipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia.”
Luka 17:20-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki. Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na mali yake imo ndani ya nyumba, asishuke ili kuitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu yeyote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na yeyote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. [ Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.] Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Luka 17:20-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki. Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. [ Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.] Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.
Luka 17:20-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu alipoulizwa na Mafarisayo Ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii, wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.” Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona. Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ Au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie. Kwa maana kama vile umeme wa radi umulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki. “Kama ilivyokuwa siku za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu. Watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote. “Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Loti: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga. Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote. “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa. Siku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote. Mkumbukeni mke wa Loti! Mtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [ Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]” Kisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana?” Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”