Luka 18:19-34
Luka 18:19-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu. Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata. Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu, asiyepokea zaidi mara nyingi katika zamani hizi, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Akawachukua wale Thenashara, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote yatatimizwa, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii. Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate; nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka. Walakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa.
Luka 18:19-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akamwambia, “Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Waheshimu baba yako na mama yako.’” Yeye akasema, “Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.” Yesu aliposikia hayo, akamwambia, “Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: Uza kila kitu ulicho nacho, wagawie maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate.” Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana. Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, “Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu! Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wale watu waliposikia hayo, wakasema, “Nani basi, atakayeokolewa?” Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu.” Naye Petro akamwuliza, “Na sisi, je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au ndugu au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na uhai wa milele wakati ujao.” Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa. Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate. Watampiga mijeledi na kumuua; lakini siku ya tatu atafufuka.” Lakini wao hawakuelewa jambo hilo hata kidogo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.
Luka 18:19-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni rahisi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu. Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata. Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu, asiyepokea zaidi mara nyingi katika wakati huu, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Akawachukua wale Kumi na Wawili, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii yatatimizwa. Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate; nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka. Lakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa.
Luka 18:19-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ” Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.” Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.” Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!” Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.” Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa. Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. Naye siku ya tatu atafufuka.” Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.