Luka 18:9-17
Luka 18:9-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia mfano huu watu waliojiamini ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea. Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambia, Mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.
Luka 18:9-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea. Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambia, Mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.
Luka 18:9-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine. “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: Mmoja Mfarisayo, na mwingine mtozaushuru. Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: ‘Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: Walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtozaushuru. Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.’ Lakini yule mtozaushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: ‘Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.’ Nawaambieni, huyu mtozaushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.” Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali. Lakini Yesu akawaita kwake akisema: “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika ufalme huo.”
Luka 18:9-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’ “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’ “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.” Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea. Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”