Luka 19:28-40
Luka 19:28-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu. Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia: “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwanapunda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungueni, mkamlete hapa. Kama mtu akiwauliza kwa nini mnamfungua, mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’” Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia. Walipokuwa wanamfungua yule mwanapunda, wenyewe wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua mwanapunda huyu?” Nao wakawajibu, “Bwana anamhitaji.” Basi, wakampelekea Yesu yule mwanapunda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake, wakampandisha Yesu juu yake. Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani. Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; wakawa wanasema: “Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!” Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!” Yesu akawajibu, “Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti.”
Luka 19:28-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu. Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa. Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda? Wakasema, Bwana ana haja naye. Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.
Luka 19:28-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu. Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, akisema, Nendeni mpaka katika kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwanapunda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu yeyote bado, mfungueni mkamlete hapa. Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. Na walipokuwa wakimfungua mwanapunda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwanapunda? Wakasema, Bwana anamhitaji. Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwanapunda, wakampandisha Yesu. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. Na alipokuwa amekaribia mteremko wa mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatanena kwa sauti kuu.
Luka 19:28-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya Yesu kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu. Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima uitwao Mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ” Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama vile Yesu alivyokuwa amewaambia. Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?” Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.” Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake. Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani. Alipokaribia mahali yanapoanzia materemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema: “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa Jina la Bwana!” “Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwamo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.” Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”