Luka 2:22-35 - Linganisha Matoleo Yote
Luka 2:22-35 BHN (Biblia Habari Njema)
Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana. Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.” Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana. Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria, Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema: “Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, umruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta, ambao umeutayarisha uonekane na watu wote: Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli.” Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.”
Luka 2:22-35 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.
Luka 2:22-35 SRUV (Swahili Revised Union Version)
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo Torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto wa kiume aliye kifungua mimba wa mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.
Luka 2:22-35 NEN (Neno)
Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Sheria ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda wawili wa njiwa”. Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema: “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi, sasa mruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako, ulioweka tayari machoni pa watu wote, nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.” Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”