Luka 22:26-38
Luka 22:26-38 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. Kwa maana, ni nani aliye mkuu: Yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. “Nyinyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi ufalme, vivyo hivyo nami ninawakabidhi nyinyi ufalme. Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu na kuketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. “Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta nyinyi kama mtu anavyopepeta ngano. Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.” Naye Petro akamjibu, “Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa.” Yesu akamjibu, “Nakuambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, “Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?” Wakajibu, “La.” Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: ‘Aliwekwa kundi moja na wahalifu,’ ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.” Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!”
Luka 22:26-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isipungue; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho lake akanunue. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.
Luka 22:26-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.
Luka 22:26-38 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye anayetawala na awe kama yeye anayehudumu. Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule anayeketi mezani au ni yule anayehudumu? Si ni yule aliyeketi mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule anayehudumu. Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, nami ninawapa ninyi, ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya utawala, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.” Isa akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe baada ya kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.” Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata katika kifo.” Isa akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba unanijua.” Kisha Isa akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.” Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe kunihusu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu hayana budi kutimizwa.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.”