Luka 4:38-43
Luka 4:38-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa.
Luka 4:38-43 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia. Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walijua kwamba yeye ndiye Kristo. Kesho yake asubuhi, Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta. Hao watu walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.”
Luka 4:38-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akainuka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafutatafuta, na walipomfikia, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana nilitumwa kwa sababu hiyo.
Luka 4:38-43 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie. Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka saa ile ile, naye akaanza kuwahudumia. Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Yesu watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya. Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Kristo. Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke. Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”