Luka 6:1-11
Luka 6:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusapukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao. Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kulia umepooza. Na Waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kama ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.
Luka 6:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao. Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.
Luka 6:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.” Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
Luka 6:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ikawa siku moja ya Sabato Yesu alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake. Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa? Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.” Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Ikawa siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia ndani ya sinagogi na akawa anafundisha. Huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu. Kwa hivyo wakawa wanamwangalia sana ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato. Lakini Yesu alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka usimame mbele ya watu wote.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote. Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?” Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha na mkono wake ukaponywa kabisa. Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao ni nini watakachomtendea Yesu.