Mathayo 10:24-33
Mathayo 10:24-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake. Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake! “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinongʼonwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi. “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”
Mathayo 10:24-33 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumishi hampiti bwana wake. Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je, hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi? “Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. Ninalowaambieni nyinyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinongonezwa, litangazeni hadharani. Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Kwa hiyo msiogope; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi. “Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
Mathayo 10:24-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika Jehanamu. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Mathayo 10:24-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.