Mathayo 13:1-17
Mathayo 13:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa. Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashuani, akaketi. Watu wote walisimama kwenye ukingo wa ziwa, naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, ziliteketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga. Nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: Nyingine punje mia, nyingine sitini na nyingine thelathini. Mwenye masikio na asikie!” Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: ‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa. Kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’ “Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.
Mathayo 13:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda katika mashua, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Na alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; zikaota haraka, kwa kukosa udongo wenye kina; Lakini jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie. Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
Mathayo 13:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.” Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao hawajapewa. Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano: “Ingawa wanatazama, hawaoni; wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama lakini hamtaona. Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’ Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.
Mathayo 13:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie. Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.