Mathayo 13:24-30
Mathayo 13:24-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana. Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’ Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayangoe?’ Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia. Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’”
Mathayo 13:24-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.
Mathayo 13:24-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.
Mathayo 13:24-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea. “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’ “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’ “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”