Mathayo 14:13-21
Mathayo 14:13-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao. Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na saa za mchana zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Si lazima waende, wapeni nyinyi chakula.” Lakini wao wakamwambia, “Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili.” Yesu akawaambia, “Nileteeni hapa.” Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.
Mathayo 14:13-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika mashua, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
Mathayo 14:13-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao. Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.” Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.” Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” Yesu akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia makutano. Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.
Mathayo 14:13-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.