Mathayo 14:22-33
Mathayo 14:22-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ngambo ya ziwa wakati yeye anayaaga makundi ya watu. Baada ya kuwaaga watu, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, na wakati huo ile mashua ilikwisha fika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikumbwa na taabu kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliogopa sana, wakasema, “Ni mzimu!” Wakapiga yowe kwa hofu. Mara, Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Petro akamwambia, “Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako.” Yesu akasema, “Haya, njoo.” Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, “Bwana, niokoe!” Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, “Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?” Kisha wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.”
Mathayo 14:22-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande katika mashua na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na ile mashua imekwisha kufika katikati ya bahari, inapigwa sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa unawakabili. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni mzimu; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka katika mashua, akatembea juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda katika mashua, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya mashua wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.
Mathayo 14:22-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.
Mathayo 14:22-33 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wamtangulie kwenda ng’ambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiaga ule umati. Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Isa alikuwa huko peke yake. Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Isa akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa. Lakini mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.” Petro akamjibu, “Bwana Isa, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.” Isa akamwambia, “Njoo.” Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Isa. Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, akapaza sauti na kusema, “Bwana, niokoe!” Mara Isa akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?” Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Isa, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”