Mathayo 14:22-36
Mathayo 14:22-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande katika mashua na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na ile mashua imekwisha kufika katikati ya bahari, inapigwa sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa unawakabili. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni mzimu; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka katika mashua, akatembea juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda katika mashua, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya mashua wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa wagonjwa; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.
Mathayo 14:22-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa hawawezi; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.
Mathayo 14:22-36 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake. Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa. Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.” Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.” Yesu akamwambia, “Njoo.” Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!” Mara Yesu akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?” Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Yesu, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti. Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote, wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.
Mathayo 14:22-36 Biblia Habari Njema (BHN)
Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ngambo ya ziwa wakati yeye anayaaga makundi ya watu. Baada ya kuwaaga watu, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, na wakati huo ile mashua ilikwisha fika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikumbwa na taabu kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliogopa sana, wakasema, “Ni mzimu!” Wakapiga yowe kwa hofu. Mara, Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Petro akamwambia, “Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako.” Yesu akasema, “Haya, njoo.” Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, “Bwana, niokoe!” Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, “Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?” Kisha wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.” Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.