Mathayo 20:29-34
Mathayo 20:29-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata. Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Bwana, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.” Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.
Mathayo 20:29-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Walipokuwa wakitoka Yeriko mkutano mkubwa wakamfuata. Na tazama, vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya njia, nao waliposikia ya kwamba Yesu anapita, walipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi! Mkutano wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi! Yesu akasimama, akawaita, akasema, Mnataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Bwana, twataka macho yetu yafumbuliwe. Yesu akawahurumia, akawagusa macho yao; mara wakapata kuona, wakamfuata.
Mathayo 20:29-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata walipokuwa wakitoka Yeriko mkutano mkubwa wakamfuata. Na tazama, vipofu wawili wameketi kando ya njia, nao waliposikia ya kwamba Yesu anapita, walipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi! Mkutano wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi! Yesu akasimama, akawaita, akasema, Mnataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Bwana, twataka macho yetu yafumbuliwe. Yesu akawahurumia, akawagusa macho yao; mara wakapata kuona, wakamfuata.
Mathayo 20:29-34 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Isa na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu wakamfuata. Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Isa alikuwa anapita, wakapaza sauti wakisema, “Bwana Isa, Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Umati wa watu wakawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana Isa, Mwana wa Daudi, tuhurumie.” Isa akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.” Isa akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.