Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 21:23-32

Mathayo 21:23-32 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu aliingia hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?” Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu,’ tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.” Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. “Nyinyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi. Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini. Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.” Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.”

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:23-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha na kusema, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka hayo?” Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Kama mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. Ubatizo wa Yohana, ulitoka wapi? Je, ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?” Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.” Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.” “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda. “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda, bwana,’ lakini hakwenda. “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?” Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.” Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu. Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.

Shirikisha
Soma Mathayo 21