Mathayo 23:23-28 - Linganisha Matoleo Yote
Mathayo 23:23-28 BHN (Biblia Habari Njema)
Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine. Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia! “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyanganyi na uchoyo. Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu. Hali kadhalika nyinyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
Mathayo 23:23-28 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)
Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.
Mathayo 23:23-28 SRUV (Swahili Revised Union Version)
Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nako kupate kuwa safi. Ole wenu, Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.
Mathayo 23:23-28 NEN (Neno)
“Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo. Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia! “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia. “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.