Mathayo 24:1-14
Mathayo 24:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alitoka hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonesha majengo ya hekalu. Yesu akawaambia, “Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.” Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?” Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watatokea wakisema kila mmoja kwamba yeye ndiye Kristo nao watawapotosha watu wengi. Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi. Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto. “Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa sababu ya jina langu. Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi. Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.
Mathayo 24:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na tetesi za vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa uchungu. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapunguka. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena Habari Njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
Mathayo 24:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
Mathayo 24:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu. Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.” Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?” Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi. Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu. “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.