Mathayo 26:36-45
Mathayo 26:36-45 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.” Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko. Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.” Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda tena mara ya pili akasali: “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.” Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi.
Mathayo 26:36-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniondokee; lakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho iko radhi, lakini mwili ni dhaifu. Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniondokee nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yalijawa na usingizi. Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi.
Mathayo 26:36-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito. Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi.
Mathayo 26:36-45 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.” Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.” Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.” Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.” Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale. Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.