Mathayo 3:1-10
Mathayo 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku zile Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea: “Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: “Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka pande zote za Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja? Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msifikiri na kujisemea, ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.
Mathayo 3:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Yudea, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Ndipo walipomwendea wa Yerusalemu, na wa Yudea wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. Na alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazawa wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Abrahamu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Abrahamu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
Mathayo 3:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
Mathayo 3:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema: “Sauti ya mtu aliaye huko nyikani, ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.’ ” Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka kwa mawe haya. Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.