Marko 11:1-11
Marko 11:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwanapunda amefungwa, ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnafanya hivyo?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.’” Basi, wakaenda, wakamkuta mwanapunda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwanapunda?” Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. Wakampelekea Yesu huyo mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwanapunda na Yesu akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. Watu wote waliotangulia na wale waliofuata, wakapaza sauti zao wakisema, “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Ubarikiwe ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Sifa kwa Mungu juu mbinguni!” Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
Marko 11:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa. Wakaenda zao, wakamwona mwanapunda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwanapunda? Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu. Wakamletea Yesu yule mwanapunda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni. Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Kumi na Wawili.
Marko 11:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa. Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda? Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu. Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni. Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara.
Marko 11:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ” Wakaenda, wakamkuta mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana-punda?” Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!” “Hosana kwake yeye aliye juu!” Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.