Marko 15:1-20
Marko 15:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, waalimu wa sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato. Pilato akamwuliza Yesu, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.” Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi. Pilato akamwuliza tena Yesu, “Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako.” Lakini Yesu hakujibu neno, hata Pilato akashangaa. Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji. Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake. Pilato akawauliza, “Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?” Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu. Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba. Pilato akawauliza tena, “Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Watu wote wakapaza sauti tena: “Msulubishe!” Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini! Amefanya ubaya gani?” Lakini wao wakazidi kupaza sauti, “Msulubishe!” Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe. Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani. Wakaanza kumsalimu, “Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia. Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
Marko 15:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, aliyefungwa pamoja na waasi, waliosababisha mauaji katika uhalifu huo. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. Lakini wakuu wa makuhani wakawachochea watu, kuwa afadhali awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? Wakapiga kelele tena, Msulubishe. Pilato akawaambia, Kwani ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulubishe. Pilato kwa kupenda kuwaridhisha watu, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulubiwe. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, makao makuu ya mtawala), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani; wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakampeleka nje ili wamsulubishe.
Marko 15:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? Wakapiga kelele tena, Msulibishe. Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe. Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani; wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.
Marko 15:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato. Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.” Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.” Lakini Yesu hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa. Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka. Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake. Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?” Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu. Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake. Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulubishe!” Pilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe. Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari. Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani. Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki. Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.