Marko 15:33-41
Marko 15:33-41 Biblia Habari Njema (BHN)
Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa giza likaikumba nchi yote. Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, “Sikiliza! Anamwita Elia.” Mtu mmoja akakimbia, akaichovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, “Hebu tuone kama Elia atakuja kumteremsha msalabani!” Yesu akapaza sauti kubwa, akakata roho. Basi, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini. Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake alipoona kwamba Yesu alikata roho namna hiyo, akasema, “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalene, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye.
Marko 15:33-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hadi saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumteremsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini. Basi yule kamanda, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.
Marko 15:33-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini. Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.
Marko 15:33-41 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa. Mnamo saa tisa, Yesu akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Eliya.” Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.” Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini. Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome. Hawa walifuatana na Yesu na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwepo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu.