Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 5:21-43

Marko 5:21-43 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa. Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi aitwaye Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake, akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu na kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi.” Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande. Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake. Alifanya hivyo, maana alijisemea, “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.” Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake. Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, “Nani aliyegusa mavazi yangu?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona unauliza nani aliyekugusa?” Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo. Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.” Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?” Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, “Usiogope, amini tu.” Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi. Akaingia ndani, akawaambia, “Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu.” Lakini wao wakamcheka. Basi, akawatoa wote nje, akawachukua baba yake na mama yake huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana. Kisha akamshika mkono, akamwambia, “Talitha, kumi,” maana yake, “Msichana, nakuambia, amka!” Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi. Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.

Shirikisha
Soma Marko 5

Marko 5:21-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng'ambo katika ile mashua, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yuko karibu kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye; mkutano mkuu wakamfuata, wakimsongasonga. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuvumilia mateso mengi kutoka kwa matabibu wengi, na kugharimiwa mali yake yote aliyokuwa nayo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. Aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, huku akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusongasonga, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza ukweli wote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, nenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwa nini uzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.

Shirikisha
Soma Marko 5

Marko 5:21-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye; mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga-songa. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula. a.

Shirikisha
Soma Marko 5

Marko 5:21-43 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ngʼambo, umati mkubwa wa watu ukamzunguka yeye akiwa hapo kando ya bahari. Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Yesu, akapiga magoti miguuni pake, akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye atakuwa hai.” Hivyo Yesu akaenda pamoja naye. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, nao watu wakawa wanamsonga. Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya. Alikuwa amesikia habari za Yesu, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitaponywa.” Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa. Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’  ” Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.” Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?” Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.” Hakumruhusu mtu mwingine yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo. Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.” Wale watu wakamcheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto. Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake ni, “Msichana, nakuambia: amka!”) Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.

Shirikisha
Soma Marko 5