Obadia 1:15-21
Obadia 1:15-21 Biblia Habari Njema (BHN)
“Siku inakaribia ambapo mimi Mwenyezi-Mungu nitayahukumu mataifa yote. Kama mlivyowatendea wengine, ndivyo mtakavyotendewa, mtalipwa kulingana na matendo yenu. Maana, kama walivyokunywa kikombe cha ghadhabu yangu kwenye mlima wangu mtakatifu ndivyo na mataifa jirani yatakavyokunywa; watakunywa na kupepesuka, wataangamia kana kwamba hawakuwahi kuwapo duniani. “Lakini mlimani Siyoni watakuwapo wale waliosalimika nao utakuwa mlima mtakatifu. Wazawa wa Yakobo wataimiliki tena nchi iliyokuwa yao. Wazawa wa Yakobo watakuwa kama moto na wazawa wa Yosefu kama miali ya moto. Watawaangamiza wazawa wa Esau kama vile moto uteketezavyo mabua makavu, asinusurike hata mmoja wao. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema. Wale wanaokaa Negebu wataumiliki mlima Esau; wale wanaokaa Shefela wataimiliki nchi ya Wafilisti. Waisraeli watamiliki nchi za Efraimu na Samaria na watu wa Benyamini wataimiliki nchi ya Gileadi. Waisraeli walio uhamishoni Hala wataimiliki Foinike hadi Sarepta. Watu wa Yerusalemu walio uhamishoni Sefaradi wataimiliki miji ya Negebu. Waokoaji watapanda juu ya mlima Siyoni ili kuutawala mlima Esau; naye Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye Mfalme.”
Obadia 1:15-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe. Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kuyumbayumba, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe. Bali katika mlima Sayuni kutakuwa na watakaookoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki tena milki zao. Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa muali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo. Na watu wa Negebu wataumiliki mlima wa Esau; na watu wa Shefela watawamiliki Wafilisti; nao wataimiliki nchi ya Efraimu, na nchi ya Samaria, na Benyamini atamiliki Gileadi. Na watu wa jeshi hili la wana wa Israeli waliotekwa, walio kati ya Wakanaani, watamiliki mpaka Sarepta; na hao watu wa Yerusalemu waliotekwa, waliomo Sefaradi, wataimiliki miji ya Negebu. Tena waokoaji watakwea juu ya mlima Sayuni ili kuuhukumu mlima wa Esau; na huo ufalme utakuwa ni mali ya BWANA.
Obadia 1:15-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe. Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kubabaika, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe. Bali katika mlima Sayuni watakuwako wenye kuokoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki milki zao. Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo. Na watu wa Negebu wataumiliki mlima wa Esau; na watu wa Shefela watawamiliki Wafilisti; nao watalimiliki konde la Efraimu, na konde la Samaria, na Benyamini atamiliki Gileadi. Na watu wa jeshi hili la wana wa Israeli waliotekwa, walio kati ya Wakanaani, watamiliki mpaka Sarepta; na hao watu wa Yerusalemu waliotekwa, waliomo Sefaradi, wataimiliki miji ya Negebu. Tena waokozi watakwea juu ya mlima Sayuni ili kuuhukumu mlima wa Esau; na huo ufalme utakuwa ni mali ya BWANA.
Obadia 1:15-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Siku ya BWANA iko karibu kwa mataifa yote. Kama ulivyofanya, nawe utafanyiwa vivyo hivyo, matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako. Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo, watakunywa na kunywa, nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo. Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwepo na wale watakaookoka; nao utakuwa mtakatifu, nayo nyumba ya Yakobo itamiliki urithi wake. Nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yosefu itakuwa mwali wa moto; nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu, nao wataiwasha moto na kuiteketeza. Hakutakuwa na watakaosalimika kutoka nyumba ya Esau.” BWANA amesema. Watu kutoka nchi ya Negebu wataikalia milima ya Esau, na watu kutoka miteremko ya vilima watamiliki nchi ya Wafilisti. Watayakalia mashamba ya Efraimu na Samaria, naye Benyamini atamiliki Gileadi. Kundi la Waisraeli walioko uhamishoni Kanaani watarudi na kumiliki nchi mpaka Sarepta. Walioko uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu watamiliki miji ya Negebu. Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni kutawala milima ya Esau. Nao ufalme utakuwa wa BWANA.