Filemoni 1:1-7
Filemoni 1:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi, na kwa Afia, dada yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; naomba ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nilikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu.
Filemoni 1:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu, na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu, maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.
Filemoni 1:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi, na kwa Afia, ndugu yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu.
Filemoni 1:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu: Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu, kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako: Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo. Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.