Wafilipi 4:1-9
Wafilipi 4:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, ninaotamani sana kuwaoneni, nyinyi mlio furaha yangu na taji ya ushindi wangu, ndivyo basi mnavyopaswa kukaa imara katika kuungana na Bwana, enyi wapenzi wangu. Euodia na Suntike, nawaombeni na kuwasihi mpatane kama ndugu katika Bwana. Nawe ndugu yangu mwaminifu, nakutaka uwasaidie akina mama hao, kwani wamefanya kazi ya kueneza Injili kwa bidii pamoja nami na Klementi na wafanyakazi wenzangu wengine wote ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uhai. Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: Furahini! Upole wenu ujulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu. Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Tekelezeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu; mambo mliyosikia nimesema na kuona nimeyatenda. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi.
Wafilipi 4:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji langu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu. Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nataka na wewe pia, mtumwa mwenzangu wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliofanya kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yuko karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya heshima, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
Wafilipi 4:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu. Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
Wafilipi 4:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu. Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.