Methali 1:1-19
Methali 1:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli. Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu; kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili. Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari; mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia. Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao. Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako, Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako. Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu; Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni. Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka. Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika. Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao. Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu. Kwa kuwa mtego hutegwa bure, Mbele ya macho ya ndege ye yote. Na hao hujiotea damu yao wenyewe, Hujinyemelea nafsi zao wenyewe. Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo.
Methali 1:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Hizi ni methali za Solomoni mfalme wa Israeli, mwana wa Daudi. Methali hizi zawapatia watu hekima na nidhamu; zawafanya waelewe maneno ya busara, zawafanya kuwa na nidhamu, utaratibu, uadilifu, haki na kutenda kwa usawa. Huwapatia wajinga werevu na vijana maarifa na hadhari. Mwenye hekima azisikie na kuongeza elimu yake, naye mwenye busara apate mwongozo. Mtu aelewe methali na mifano, maneno ya wenye hekima na vitendawili vyao. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyapuuze mafundisho ya mama yako; hayo yatakupamba kilemba kichwani pako, kama mkufu shingoni mwako. Mwanangu, usikubali kushawishiwa na wenye dhambi. Wakisema: “Twende tukamvizie mtu na kumuua; njoo tukawashambulie wasio na hatia! Tutawameza kama Kuzimu wakiwa hai, watakuwa kama wale washukao Shimoni. Tutajitwalia mali zote za thamani, nyumba zetu tutazijaza nyara. Njoo ushirikiane nasi, vyote tutakavyopata tutagawana.” Wewe mwanangu usiandamane nao, uzuie mguu wako usifuatane nao. Maana wao wako mbioni kutenda maovu, haraka zao zote ni za kumwaga damu. Mtego utegwao huku ndege anaona, mtego huo wategwa bure. Wao huvizia na kujiangamiza wao wenyewe, hutega mtego wa kujinasa wao wenyewe. Ndivyo zilivyo njia za waishio kwa ukatili; ukatili huyaangamiza maisha ya wakatili.
Methali 1:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli. Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu; kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili. Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na tahadhari; mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia. Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao. Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako, Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako. Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu; Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni. Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka. Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote kwa shirika. Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao. Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu. Kwa kuwa mtego hutegwa bure, Mbele ya macho ya ndege yeyote. Na hao hujiotea damu yao wenyewe, Hujinyemelea nafsi zao wenyewe. Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo.
Methali 1:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli: Kwa kupata hekima na nidhamu; kwa kufahamu maneno ya busara; kwa kujipatia nidhamu na busara, kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea; huwapa busara wajinga, maarifa na akili kwa vijana; wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao, wenye kupambanua na wapate mwongozo; kwa kufahamu mithali na mifano, misemo na vitendawili vya wenye hekima. Kumcha BWANA ndicho chanzo cha maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako. Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako, na mkufu wa kuipamba shingo yako. Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi, usikubaliane nao. Kama wakisema, “Twende tufuatane; tukamvizie mtu na kumwaga damu, njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia; tuwameze wakiwa hai kama kaburi, wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni. Tutapata aina zote za vitu vya thamani na kujaza nyumba zetu kwa nyara. Njoo ushirikiane nasi, vitu vyote tutakavyopata tutagawana.” Mwanangu, usiandamane nao. Usiweke mguu wako katika njia zao, kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni wepesi kumwaga damu. Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu wakati ndege wote wanakuona! Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe; hujivizia tu wenyewe! Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye mali.