Methali 25:18-28
Methali 25:18-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali. Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka. Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi; Ni kama siki juu ya magadi. Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na BWANA atakupa thawabu. Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu. Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali. Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya Ni kama chemchemi iliyochafuka, Na kisima kilichokanyagwa. Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu. Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.
Methali 25:18-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtu atoaye ushahidi wa uongo dhidi ya mwenziwe, ni hatari kama rungu, upanga au mshale mkali. Kumtegemea mtu asiyeaminika wakati wa taabu, ni kama jino bovu au mguu ulioteguka. Kumwimbia mtu mwenye huzuni, ni kama kuvua nguo wakati wa baridi, au kutia siki katika kidonda. Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe maji ya kunywa. Hivyo utafanya apate aibu kali, kama makaa ya moto kichwani pake, naye Mwenyezi-Mungu atakutuza. Upepo wa kusi huleta mvua, hali kadhalika masengenyo huleta chuki. Afadhali kuishi pembeni juu ya paa, kuliko kuishi nyumbani pamoja na mwanamke mgomvi. Kama vile maji baridi kwa mwenye kiu, ndivyo habari njema kutoka mbali. Mwadilifu akubaliye kufuata mambo ya mwovu, ni chemchemi iliyochafuliwa au kisima kilichotibuliwa. Si vizuri kula asali nyingi mno; kadhalika haifai kujipendekeza mno. Mtu asiyeweza kuzuia hasira yake, ni kama mji usio na ulinzi unaposhambuliwa.
Methali 25:18-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali. Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka. Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi; Ni kama siki juu ya magadi. Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na BWANA atakupa thawabu. Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu. Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali. Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya Ni kama chemchemi iliyochafuka, Na kisima kilichokanyagwa. Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu. Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.
Methali 25:18-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kama vile rungu au upanga au mshale mkali ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake. Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa, ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida. Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi, au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito. Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale; kama ana kiu, mpe maji anywe. Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake, naye BWANA atakupa thawabu. Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua, ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira. Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi. Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali. Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au kisima kilichotiwa taka ndivyo alivyo mtu mwenye haki akishiriki na waovu. Si vyema kula asali nyingi sana, wala si heshima kujitafutia heshima yako mwenyewe. Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka ndivyo alivyo mtu ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.