Methali 26:22-28
Methali 26:22-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo; hushuka mpaka ndani kabisa tumboni. Kama rangi angavu iliyopakwa kigae, ndivyo yalivyo maneno matamu yenye nia mbaya. Mwenye chuki huficha chuki yake kwa maneno mazuri, lakini huwa ana hila moyoni mwake. Akiongea vizuri usimwamini, moyoni mwake mna chuki chungu nzima. Huenda akaficha chuki yake, lakini nia zake mbaya zitajulikana kwa wote. Amchimbiaye mwenzake shimo, hutumbukia mwenyewe; abingirishaye jiwe litamrudia mwenyewe. Asemaye uongo huwachukia hao anaowaumiza, naye abembelezaye huleta maangamizi.
Methali 26:22-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Midomo ijipendekezayo pamoja na moyo mbaya Ni kama kigae kilichofunikizwa taka za fedha. Achukiaye huficha chuki kwa midomo yake; Naye huweka akiba ya hila moyoni mwake. Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake. Ingawa chuki hufunikwa na hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko. Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia. Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.
Methali 26:22-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Midomo ijipendekezayo pamoja na moyo mbaya Ni kama kigae kilichofunikizwa taka za fedha. Achukiaye huficha chuki kwa midomo yake; Naye huweka akiba ya hila moyoni mwake. Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake. Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko. Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia. Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.
Methali 26:22-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu. Kama rangi ingʼaayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya. Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake, lakini moyoni mwake huficha udanganyifu. Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini, kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake. Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu, lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko. Kama mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake, kama mtu akivingirisha jiwe, litamrudia. Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza, nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.