Methali 31:1-9
Methali 31:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Maneno ya mfalme Lemueli. Mawaidha aliyofundishwa na mama yake: Nikuambie nini mwanangu? Nikuambie nini mwanangu niliyekuzaa? Nikuambie nini wewe niliyekuomba kwa Mungu? Usimalize nguvu zako kwa wanawake, usiwape mali yako hao wanaoangamiza wafalme. Haifai ee Lemueli, haifai wafalme kunywa divai, wala wakuu kutamani vileo. Wakinywa watasahau maagizo ya sheria, na kuwanyima haki wenye taabu. Mpe kileo mtu anayekufa, wape divai wale wenye huzuni tele; wanywe na kusahau umaskini wao, wasikumbuke tena taabu yao. Lakini wewe, lazima useme kwa ajili ya wote walio bubu; na kutetea haki za wote wasiojiweza. Sema kwa ajili yao na kuamua kwa haki, linda haki za maskini na fukara.
Methali 31:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake. Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu? Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wanaowaharibu wafalme. Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Kiko wapi kileo? Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni. Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini. Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake. Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao.
Methali 31:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake. Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu? Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme. Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo? Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni. Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini. Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake. Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao.
Methali 31:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha: “Ee mwanangu, ee mwana wa tumbo langu, ee mwana wa nadhiri zangu, Usitumie nguvu zako kwa wanawake, uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme. “Ee Lemueli, haifai wafalme, haifai wafalme kunywa mvinyo, haifai watawala kutamani sana kileo, wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru na kuwanyima haki zao wote walioonewa. Wape kileo wale wanaoangamia, mvinyo wale walio na uchungu, Wanywe na kusahau umaskini wao na wasikumbuke taabu yao tena. “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea, kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa. Sema na uamue kwa haki, tetea haki za maskini na wahitaji.”