Methali 31:10-19
Methali 31:10-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Mke mwema kweli, apatikana wapi? Huyo ana thamani kuliko johari! Mumewe humwamini kwa moyo, kwake atapata faida daima. Kamwe hamtendei mumewe mabaya, bali humtendea mema maisha yake yote. Hutafuta sufu na kitani, na kufanya kazi kwa mikono yake kwa bidii. Yeye ni kama meli za biashara: Huleta chakula chake kutoka mbali. Huamka kabla ya mapambazuko, akaitayarishia jamaa yake chakula, na kuwagawia kazi watumishi wake. Hufikiria kununua shamba, kisha hulinunua, na kulima zabibu kwa faida ya jasho lake. Huwa tayari kufanya kazi kwa nguvu na kuiimarisha mikono yake. Hutambua kwamba shughuli zake zina faida; hufanya kazi hata usiku kwa mwanga wa taa yake. Husokota nyuzi kwa mikono yake mwenyewe, kwa vidole vyake mwenyewe husuka nguo zake.
Methali 31:10-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana thamani yake yapita thamani ya marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake. Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake kwa moyo wote. Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali. Tena huamka, kabla usiku haujaisha; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao. Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu. Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu. Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku. Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.
Methali 31:10-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake. Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo. Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali. Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao. Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu. Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu. Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku. Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.
Methali 31:10-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata? Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani. Mume wake anamwamini kikamilifu wala hakosi kitu chochote cha thamani. Humtendea mumewe mema, wala si mabaya, siku zote za maisha yake. Huchagua sufu na kitani naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii. Yeye ni kama meli za biashara akileta chakula chake kutoka mbali. Yeye huamka kungali bado giza huwapa jamaa yake chakula na mafungu kwa watumishi wake wa kike. Huangalia shamba na kulinunua, kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu. Hufanya kazi zake kwa nguvu, mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake. Huona kwamba biashara yake ina faida, wala taa yake haizimiki usiku. Huweka mikono yake kwenye pia, navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.