Methali 6:20-35
Methali 6:20-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, wala usisahau mafundisho ya mama yako; yaweke daima moyoni mwako, yafunge shingoni mwako. Yatakuongoza njiani mwako, yatakulinda wakati ulalapo, yatakushauri uwapo macho mchana. Maana amri hiyo ni taa, na sheria hiyo ni mwanga. Maonyo hayo na nidhamu yatuweka njiani mwa uhai. Yatakulinda mbali na mwanamke mbaya, yatakuepusha na maneno matamu ya mwanamke mgeni. Usimtamani mwanamke huyo kwa uzuri wake, wala usikubali kunaswa kwa kope za macho yake. Mtu hupoteza kipande cha mkate kwa malaya, lakini kwa mke wa mtu mwingine utapoteza uhai wako wote. Je, waweza kuweka moto kifuani na nguo zako zisiungue? Je, waweza kukanyaga makaa ya moto na nyayo zako zisiungue? Ndivyo alivyo mwanamume alalaye na mke wa mwenzake; yeyote anayemgusa mwanamke huyo hataacha kuadhibiwa. Watu hawambezi sana mtu akiiba kwa sababu ya njaa; lakini akipatikana lazima alipe mara saba; tena atatoa mali yote aliyo nayo. Mwanamume anayezini na mke wa mtu hana akili kabisa; huyo hujiangamiza yeye mwenyewe. Atapata majeraha na madharau; fedheha atakayopata haitamtoka. Maana wivu wa mume humfanya kuwa mkali kabisa; wakati atakapolipiza kisasi hana cha kuhurumia. Hatakubali fidia yoyote; wala kutulizwa na zawadi zako nyingi.
Methali 6:20-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako. Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako. Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe. Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani Je! Mtu aweza kuchukua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia. Watu hawamdharau mwizi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa; Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake. Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; Wala hatahurumia siku ya kujilipizia kisasi. Hatakubali fidia yoyote; Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.
Methali 6:20-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako. Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako. Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe. Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia. Watu hawamdharau mwivi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa; Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake. Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; Wala hatahurumia siku ya kujilipiza kisasi. Hatakubali ukombozi uwao wote; Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.
Methali 6:20-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwanangu, zishike amri za baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako. Yafunge katika moyo wako daima, yakaze kuizunguka shingo yako. Wakati utembeapo, yatakuongoza; wakati ulalapo, yatakulinda; wakati uamkapo, yatazungumza nawe. Kwa maana amri hizi ni taa, mafundisho haya ni mwanga na maonyo ya maadili ni njia ya uzima, yakikulinda na mwanamke aliyepotoka, kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka. Moyo wako usitamani uzuri wake wala macho yake yasikuteke, kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini, hata ukose kipande cha mkate, naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa. Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake bila nguo zake kuungua? Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto yanayowaka bila miguu yake kuungua? Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine; hakuna yeyote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa. Watu hawamdharau mwizi kama akiiba kukidhi njaa yake wakati ana njaa. Pamoja na hayo, kama akikamatwa, lazima alipe mara saba, ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake. Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa; yeyote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe. Mapigo na aibu ni fungu lake na aibu yake haitafutika kamwe; kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume, naye hataonyesha huruma alipizapo kisasi. Hatakubali fidia yoyote; atakataa malipo, hata yakiwa makubwa kiasi gani.