Zaburi 1:1-6
Zaburi 1:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Heri mtu asiyefuata shauri la waovu, asiyeshiriki njia za wenye dhambi, wala kujumuika na wenye dharau; bali huifurahia sheria ya Mwenyezi-Mungu, na kuitafakari mchana na usiku. Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito, unaozaa matunda kwa wakati wake, na majani yake hayanyauki. Kila afanyalo hufanikiwa. Lakini waovu sivyo walivyo; wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kwa hiyo watu waovu wataanguka wakati wa hukumu, wenye dhambi hawatakaa na kusanyiko la waadilifu. Maana Mwenyezi-Mungu huziongoza njia za waadilifu; lakini njia za waovu zitaishia katika maangamizi.
Zaburi 1:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wenye dhambi; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki. Kwa kuwa BWANA anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.
Zaburi 1:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki. Kwa kuwa BWANA anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.
Zaburi 1:1-6 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha. Bali huifurahia Torati ya Mwenyezi Mungu, naye huitafakari hiyo Torati usiku na mchana. Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa. Sivyo walivyo waovu! Wao ni kama makapi yanayopeperushwa na upepo. Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki. Kwa maana Mwenyezi Mungu huziangalia njia za mwenye haki, bali njia za waovu zitaangamia.