Zaburi 120:1-7
Zaburi 120:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, naye akanijibu. Uniokoe ee Mwenyezi-Mungu, na watu wadanganyifu na waongo. Enyi watu wadanganyifu, mtapewa kitu gani? Mtaadhibiwa namna gani? Kwa mishale mikali ya askari, kwa makaa ya moto mkali! Ole wangu kwamba naishi kama mgeni huko Mesheki; naishi kama mgeni katika mahema ya Kedari. Nimeishi muda mrefu mno kati ya watu wanaochukia amani! Wakati ninaposema nataka amani, wao wanataka tu vita.
Zaburi 120:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika shida yangu nilimlilia BWANA Naye akaniitikia. Ee BWANA, uniponye Na midomo ya uongo na ulimi wa hila. Akupe nini, akuzidishie nini, Ewe ulimi wenye hila? Mishale ya mtu hodari iliyochongoka, Pamoja na makaa ya mretemu. Ole wangu mimi! Kwa kuwa ni mgeni katika Mesheki; Na kufanya makao yangu Katikati ya hema za Kedari. Kwa muda mrefu nimeishi, Pamoja na watu wanaoichukia amani. Mimi nazingatia amani; Bali ninenapo, wao wanataka vita.
Zaburi 120:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika shida yangu nalimlilia BWANA Naye akaniitikia. Ee BWANA, uiponye nafsi yangu Na midomo ya uongo na ulimi wa hila. Akupe nini, akuzidishie nini, Ewe ulimi wenye hila? Mishale ya mtu hodari iliyochongoka, Pamoja na makaa ya mretemu. Ole wangu mimi! Kwa kuwa nimekaa katika Mesheki; Na kufanya maskani yangu Katikati ya hema za Kedari. Nafsi yangu imekaa siku nyingi, Pamoja naye aichukiaye amani. Mimi ni wa amani; Bali ninenapo, wao huelekea vita.
Zaburi 120:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika dhiki yangu namwita BWANA, naye hunijibu. Ee BWANA, uniokoe kutoka midomo ya uongo na ndimi za udanganyifu. Atakufanyia nini, au akufanyie nini zaidi, ewe ulimi mdanganyifu? Atakuadhibu kwa mishale mikali ya shujaa, kwa makaa yanayowaka ya mti wa mretemu. Ole wangu kwa kuwa naishi Mesheki, kwamba naishi katikati ya hema za Kedari! Nimeishi muda mrefu mno miongoni mwa wale wanaochukia amani. Mimi ni mtu wa amani; lakini ninaposema, wao wanataka vita.