Zaburi 121:1-8
Zaburi 121:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu hutoka kwa BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi. Hatauacha mguu wako usogezwe; Akulindaye hatasinzia; Naam, hatasinzia wala hatalala, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli katika mkono wako wa kulia. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.
Zaburi 121:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.
Zaburi 121:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia. Hatakuacha uanguke; mlinzi wako hasinzii. Kweli mlinzi wa Israeli hasinzii wala halali. Mwenyezi-Mungu ni mlinzi wako; yuko upande wako wa kulia kukukinga. Mchana jua halitakuumiza, wala mwezi wakati wa usiku. Mwenyezi-Mungu atakukinga na baya lolote; atayalinda salama maisha yako. Mwenyezi-Mungu atakulinda katika shughuli zako zote tangu sasa na hata milele.
Zaburi 121:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nayainua macho yangu nitazame vilima, msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu hutoka kwa BWANA, Muumba wa mbingu na dunia. Hatauacha mguu wako uteleze, yeye akulindaye hatasinzia, hakika, yeye alindaye Israeli hatasinzia wala hatalala usingizi. BWANA anakulinda, BWANA ni uvuli wako mkono wako wa kuume, jua halitakudhuru mchana, wala mwezi wakati wa usiku. BWANA atakukinga na madhara yote, atayalinda maisha yako, BWANA atakulinda unapoingia na unapotoka, tangu sasa na hata milele.