Zaburi 122:1-9
Zaburi 122:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nilishangilia pamoja na wale walioniambia, “Twende nyumbani ya BWANA.” Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama malangoni mwako. Yerusalemu imejengwa vyema kama mji ambao umeshikamanishwa pamoja. Huko ndiko makabila hukwea, makabila ya BWANA, kulisifu jina la BWANA kulingana na maagizo waliopewa Israeli. Huko viti vya enzi vya hukumu hukaa, viti vya enzi vya nyumba ya Daudi. Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu: “Wote wakupendao na wawe salama. Amani na iwepo ndani ya kuta zako na usalama ndani ya ngome zako.” Kwa ajili ya ndugu zangu na marafiki, nitasema, “Amani iwe ndani yako.” Kwa ajili ya nyumba ya BWANA Mungu wetu, nitatafuta mafanikio yako.
Zaburi 122:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilifurahi waliponiambia: “Twende nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.” Sasa tuko tumesimama, kwenye malango yako, ee Yerusalemu! Yerusalemu, mji uliojengwa, ili jumuiya ikutane humo. Humo ndimo makabila yanamofika, naam, makabila ya Israeli, kumshukuru Mwenyezi-Mungu kama alivyoagiza. Humo mmewekwa mahakama ya hukumu ya haki, mahakama ya ukoo wa kifalme wa Daudi. Uombeeni Yerusalemu amani: “Wote wakupendao na wafanikiwe! Ndani ya kuta zako kuwe na amani, majumbani mwako kuweko usalama!” Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu, ee Yerusalemu, nakutakia amani! Kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ninakuombea upate fanaka!
Zaburi 122:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nilifurahi waliponiambia, Twende nyumbani kwa BWANA. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu. Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana, Huko ndiko wapandako kabila, makabila ya BWANA; Kama ulivyowaamuru Waisraeli, Walishukuru jina la BWANA. Maana huko viliwekwa viti vya hukumu, Viti vya enzi vya ukoo wa Daudi. Uombeeni Yerusalemu amani; Na wafanikiwe wakupendao; Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe. Kwa ajili ya nyumba ya BWANA, Mungu wetu, Nitakuombea mema.
Zaburi 122:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu. Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana, Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za BWANA; Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la BWANA. Maana huko viliwekwa viti vya hukumu, Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. Utakieni Yerusalemu amani; Na wafanikiwe wakupendao; Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe. Kwa ajili ya nyumba ya BWANA, Mungu wetu, Nikutafutie mema.