Zaburi 138:1-8
Zaburi 138:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kwa moyo wangu wote, naimba sifa zako mbele ya miungu. Ninasujudu kuelekea hekalu lako takatifu; nalisifu jina lako, kwa sababu ya fadhili zako na uaminifu wako; kwa sababu umeweka jina lako na neno lako juu ya kila kitu. Nilipokulilia, wewe ulinijibu; umeniongezea nguvu zangu. Wafalme wote duniani watakusifu, ee Mwenyezi-Mungu, kwa sababu wameyasikia maneno yako. Wataimba sifa za matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, kwa maana utukufu wako ni mkuu. Ingawa wewe ee Mwenyezi-Mungu, uko juu ya wote, unawaangalia kwa wema walio wanyonge; nao wenye kiburi huwaona kutoka mbali. Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha. Ee Mwenyezi-Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi. Fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zadumu milele. Usisahau kazi ya mkono wako mwenyewe.
Zaburi 138:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi. Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, Nitalishukuru jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, Kwa maana umeikuza ahadi yako, na jina lako juu ya vyote. Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. Ee BWANA, wafalme wote wa dunia watakushukuru, Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako. Naam, wataziimba njia za BWANA, Kwa maana utukufu wa BWANA ni mkuu. Ingawa BWANA yuko juu, anamjali mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapopitia katika shida, Unanilinda juu ya hasira ya adui zangu, Unaunyosha mkono wako, Na mkono wako wa kulia unaniokoa. BWANA atanitimizia malengo yake kwangu; Ee BWANA, fadhili zako ni za milele; Usiiache kazi ya mikono yako.
Zaburi 138:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi. Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, Nitalishukuru jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote. Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. Ee BWANA, wafalme wote wa dunia watakushukuru, Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako. Naam, wataziimba njia za BWANA, Kwa maana utukufu wa BWANA ni mkuu. Ingawa BWANA yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa. BWANA atanitimilizia mambo yangu; Ee BWANA, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.
Zaburi 138:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nitakusifu wewe, Ee BWANA, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako juu ya vitu vyote. Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee BWANA, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. Wao na waimbe kuhusu njia za BWANA, kwa maana utukufu wa BWANA ni mkuu. Ingawa BWANA yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali. Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. BWANA atatimiza kusudi lake kwangu, Ee BWANA, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.