Zaburi 20:1-9
Zaburi 20:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. Akutumie msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kukutimizia mipango yako yote. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. BWANA akutimizie matakwa yako yote. Sasa najua kuwa BWANA amwokoa masihi wake; Atamjibu toka mbingu zake takatifu, Kwa matendo makuu ya wokovu Ya mkono wake wa kulia. Hawa wanataja magari na hawa farasi, Lakini sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu. Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama. BWANA, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo.
Zaburi 20:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni; jina la Mungu wa Yakobo likulinde. Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake; akutegemeze kutoka mlima Siyoni. Azikumbuke sadaka zako zote; azikubali tambiko zako za kuteketezwa. Akujalie unayotamani moyoni mwako, aifanikishe mipango yako yote. Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako; tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote! Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa. Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Hao watajikwaa na kuanguka; lakini sisi tutainuka na kusimama imara. Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu; utujibu wakati tunapokuomba.
Zaburi 20:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. BWANA akutimizie matakwa yako yote. Sasa najua kuwa BWANA amwokoa masihi wake; Atamjibu toka mbingu zake takatifu, Kwa matendo makuu ya wokovu Ya mkono wake wa kuume. Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu. Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama. BWANA, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo.
Zaburi 20:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA na akujibu unapokuwa katika dhiki, jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako. Na akutumie msaada kutoka patakatifu na akupatie msaada kutoka Sayuni. Na azikumbuke dhabihu zako zote, na azikubali sadaka zako za kuteketezwa. Na akujalie haja ya moyo wako, na aifanikishe mipango yako yote. Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda, tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu. BWANA na akupe haja zako zote. Sasa nafahamu kuwa BWANA humwokoa mpakwa mafuta wake, humjibu kutoka mbingu yake takatifu kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume. Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi, bali sisi tutalitumainia jina la BWANA, Mungu wetu. Wao wameshushwa chini na kuanguka, bali sisi tunainuka na kusimama imara. Ee BWANA, mwokoe mfalme! Tujibu tunapokuita!