Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 22:1-31

Zaburi 22:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)

Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Mbona uko mbali sana kunisaidia, mbali na maneno ya kilio changu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu; napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati. Hata hivyo, wewe ni mtakatifu; wewe watawala na kusifiwa na Waisraeli. Wazee wetu walikutegemea; walikutegemea, nawe ukawaokoa. Walikulilia wewe, wakaokolewa; walikutegemea, nao hawakuaibika. Lakini mimi ni mdudu tu, wala si mtu; nimepuuzwa na kudharauliwa na watu. Wote wanionao hunidhihaki; hunifyonya na kutikisa vichwa vyao. Husema: “Alimtegemea Mwenyezi-Mungu, basi, Mungu na amkomboe! Kama Mungu anapendezwa naye, basi, na amwokoe!” Lakini ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, uliniweka salama kifuani pa mama yangu. Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu. Tangu nilipozaliwa wewe umekuwa Mungu wangu. Usikae mbali nami, kwani taabu imekaribia; wala hakuna wa kunisaidia. Maadui wengi wanizunguka kama fahali; wamenisonga kama fahali wakali wa Bashani! Wanafunua vinywa vyao kama simba, tayari kushambulia na kurarua. Nimekwisha kama maji yaliyomwagika; mifupa yangu yote imeteguka; moyo wangu ni kama nta, unayeyuka ndani mwangu. Koo langu limekauka kama kigae; ulimi wangu wanata kinywani mwangu. Umeniacha kwenye mavumbi ya kifo. Genge la waovu limenizunguka; wananizingira kama kundi la mbwa; wamenitoboa mikono na miguu. Nimebaki mifupa mitupu; maadui zangu waniangalia na kunisimanga. Wanagawana nguo zangu, na kulipigia kura vazi langu. Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, usikae mbali nami; ewe msaada wangu, uje haraka kunisaidia. Iokoe nafsi yangu mbali na upanga, yaokoe maisha yangu makuchani mwa mbwa hao! Uniokoe kinywani mwa simba; iokoe nafsi yangu dhaifu toka pembe za nyati hao. Nitawasimulia ndugu zangu matendo yako; nitakusifu kati ya kusanyiko lao: Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, msifuni! Mtukuzeni enyi wazawa wote wa Yakobo! Mcheni Mungu enyi wazawa wote wa Israeli! Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge; wala hajifichi mbali naye, ila humsikia anapomwomba msaada. Kwa sababu yako ninakusifu katika kusanyiko kubwa la watu; nitatimiza ahadi zangu mbele yao wakuchao. Maskini watakula na kushiba; wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu watamsifu. Mungu awajalie kuishi milele! Ulimwengu wote utakumbuka na kumrudia Mwenyezi-Mungu; jamaa zote za mataifa zitamwabudu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mfalme; yeye anayatawala mataifa. Wenye kiburi wote duniani watasujudu mbele yake; wote ambao hufa watainama mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. Vizazi vijavyo vitamtumikia; watu watavisimulia habari za Mwenyezi-Mungu, watatangaza matendo yake ya wokovu. Watu wasiozaliwa bado wataambiwa: “Mwenyezi-Mungu ndiye aliyefanya hayo!”

Shirikisha
Soma Zaburi 22

Zaburi 22:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Lakini Wewe U Mtakatifu, Utukuzwaye na sifa za Israeli. Baba zetu walikutumainia Wewe, Walitumainia, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumainia, nao hawakuaibika. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Nimedharauliwa na kupuuzwa na watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee BWANA; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinisalimisha matitini mwa mama yangu. Kwako nilitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi. Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga; Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma. Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya moyo wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenidunga mikono na miguu. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, BWANA, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa. Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu. Ninyi mnaomcha BWANA, msifuni, Enyi nyote mlio wazawa wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazawa wa Israeli. Maana hapuuzi Wala kuchukizwa na mateso ya anayeteswa, Wala hamfichi uso wake, Bali humsikia akimlilia. Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao. Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao BWANA watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele. Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea BWANA; Jamaa zote za mataifa watamsujudia. Maana ufalme ni wa BWANA, Naye ndiye awatawalaye mataifa. Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake, Wazawa wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za BWANA, Kwa kizazi kitakachokuja, Watautangaza wokovu wake kwa watakaozaliwa, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.

Shirikisha
Soma Zaburi 22

Zaburi 22:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee BWANA; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu. Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi. Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga; Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma. Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, BWANA, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa. Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu. Ninyi mnaomcha BWANA, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli. Maana hakulidharau teso la mteswa, Wala hakuchukizwa nalo; Wala hakumficha uso wake, Bali alipomlilia akamsikia. Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao. Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao BWANA watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele. Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea BWANA; Jamaa zote za mataifa watamsujudia. Maana ufalme una BWANA, Naye ndiye awatawalaye mataifa. Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake, Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za BWANA, Kwa kizazi kitakachokuja, Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.

Shirikisha
Soma Zaburi 22

Zaburi 22:1-31 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa? Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu, hata usiku, sinyamazi. Hata hivyo umesimikwa kwenye kiti cha enzi, Wewe Uliye Mtakatifu; wewe ni sifa ya Israeli. Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao, walikutumaini nawe ukawaokoa. Walikulilia wewe na ukawaokoa, walikutegemea wewe nao hawakuaibika. Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu, wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau. Wote wanaoniona wananidhihaki; wananivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao: Wanasema, “Amtegemea Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu na amwokoe. Amkomboe basi, kwa maana anapendezwa naye.” Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee, hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu. Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu. Usiwe mbali nami, kwa maana shida iko karibu na hakuna wa kunisaidia. Mafahali wengi wamenizunguka, mafahali wa Bashani wenye nguvu wamenizingira. Simba wanaonguruma na kurarua mawindo wanapanua vinywa vyao dhidi yangu. Nimemiminwa kama maji, mifupa yangu yote imeteguka viungoni. Moyo wangu umegeuka kuwa nta, umeyeyuka ndani yangu. Nguvu zangu zimekauka kama kigae, ulimi wangu umegandamana na kaakaa la kinywa changu, kwa sababu umenilaza katika mavumbi ya kifo. Mbwa wamenizunguka, kundi la watu waovu limenizingira; wamenidunga mikono na miguu. Naweza kuhesabu mifupa yangu yote, watu wananikodolea macho na kunisimanga. Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura. Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, usiwe mbali. Ee Nguvu yangu, uje haraka unisaidie. Okoa maisha yangu na upanga, uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa. Niokoe kutoka kinywani mwa simba, niokoe kutoka pembe za nyati. Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu, katika kusanyiko nitakusifu wewe. Ninyi ambao mnamcha Mwenyezi Mungu, msifuni! Ninyi nyote wazao wa Yakobo, mheshimuni yeye! Mcheni yeye, ninyi wazao wa Israeli! Kwa maana hakupuuza wala kudharau mateso ya aliyeteswa; hakumficha uso wake bali alisikiliza kilio chake. Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa, nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wanaokucha wewe. Maskini watakula na kushiba, wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu watamsifu: mioyo yenu na iishi milele! Miisho yote ya dunia itakumbuka na kumgeukia Mwenyezi Mungu, nazo jamaa zote za mataifa zitasujudu mbele zake, kwa maana ufalme ni wa Mwenyezi Mungu naye huyatawala mataifa. Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu. Wote wanaoshuka mavumbini watapiga magoti mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. Wazao wa baadaye watamtumikia yeye; vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana. Watatangaza haki yake kwa watu ambao hawajazaliwa bado, kwa maana yeye ametenda hili.

Shirikisha
Soma Zaburi 22