Zaburi 30:1-12
Zaburi 30:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa, wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nilikulilia msaada, nawe ukaniponya. Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu; umenipa tena uhai, umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake; kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru. Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha. Mimi nilipofanikiwa, nilisema: “Kamwe sitashindwa!” Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, umeniimarisha kama mlima mkubwa. Lakini ukajificha mbali nami, nami nikafadhaika. Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu; naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu: “Je, utapata faida gani nikifa na kushuka hadi kwa wafu? Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu? Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako? Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie; ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!” Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha; umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha. Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele.
Zaburi 30:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, nitakutukuza kwa maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu. Ee BWANA, Mungu wangu, Nilikulilia ukaniponya. Umeniinua nafsi yangu, Ee BWANA, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao Shimoni. Mwimbieni BWANA zaburi, Enyi watauwa wake. Na kutoa shukrani. Kwa kukumbuka utakatifu wake. Maana ghadhabu zake ni za muda mfupi tu; Radhi yake ni ya milele. Kilio huweza kuwapo usiku, Lakini furaha huja asubuhi. Nami nilipofanikiwa nilisema, Sitaondoshwa milele. BWANA, kwa radhi yako Wewe uliuimarisha mlima wangu. Uliuficha uso wako, Nami nikafadhaika. Ee BWANA, nilikulilia Wewe, Naam, kwa BWANA niliomba dua. Mna faida gani katika damu yangu Nishukapo Shimoni? Mavumbi yatakusifu? Yatautangaza uaminifu wako? Ee BWANA, usikie, unirehemu, BWANA, uwe msaidizi wangu. Umegeuza msiba wangu kuwa ngoma; Umeniondolea huzuni yangu, kunijalia furaha tele. Ili nafsi yangu ikusifu, Wala isinyamaze. Ee BWANA, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.
Zaburi 30:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, nitakutukuza kwa maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu. Ee BWANA, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya. Umeniinua nafsi yangu, Ee BWANA, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni. Mwimbieni BWANA zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake. Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha. Nami nilipofanikiwa nalisema, Sitaondoshwa milele. BWANA, kwa radhi yako Wewe uliuimarisha mlima wangu. Uliuficha uso wako, Nami nikafadhaika. Ee BWANA, nalikulilia Wewe, Naam, kwa BWANA naliomba dua. Mna faida gani katika damu yangu Nishukapo shimoni? Mavumbi yatakusifu? Yataitangaza kweli yako? Ee BWANA, usikie, unirehemu, BWANA, uwe msaidizi wangu. Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha. Ili utukufu wangu ukusifu, Wala usinyamaze. Ee BWANA, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.
Zaburi 30:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nitakutukuza wewe, Ee BWANA, kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi, na hukuacha adui zangu washangilie juu yangu. Ee BWANA, Mungu wangu, nilikuita unisaidie na wewe umeniponya. Ee BWANA, umenitoa Kuzimu, umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti. Mwimbieni BWANA, enyi watakatifu wake; lisifuni jina lake takatifu. Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi, bali upendo wake hudumu siku zote. Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha, lakini asubuhi kukawa na furaha. Nilipofanikiwa nilisema, “Sitatikiswa kamwe.” Ee BWANA, uliponijalia, uliuimarisha mlima wangu, lakini ulipouficha uso wako nilifadhaika. Kwako wewe, Ee BWANA, niliita, kwa Bwana niliomba rehema: “Kuna faida gani katika kuangamia kwangu? Katika kushuka kwangu shimoni? Je, mavumbi yatakusifu? Je, yatatangaza uaminifu wako? Ee BWANA, unisikie na kunihurumia, Ee BWANA, uwe msaada wangu.” Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza, ulinivua nguo za gunia ukanivika shangwe, ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya. Ee BWANA Mungu wangu, nitakushukuru milele.