Zaburi 33:1-12
Zaburi 33:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu! Kumsifu Mungu ni wajibu wa watu wanyofu. Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa zeze; mwimbieni kwa kinubi cha nyuzi kumi. Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kinubi vizuri na kushangilia. Neno la Mwenyezi-Mungu ni la kweli; na matendo yake yote ni ya kuaminika. Mungu apenda uadilifu na haki, dunia imejaa fadhili za Mwenyezi-Mungu. Mbingu ziliumbwa kwa neno la Mwenyezi-Mungu, na vyote vilivyomo kwa pumzi ya mdomo wake. Alikusanya maji ya bahari kama katika chupa, vilindi vya bahari akavifunga ghalani. Dunia yote na imwogope Mwenyezi-Mungu! Wakazi wote duniani, wamche! Maana alisema na ulimwengu ukawako; alitoa amri nao ukajitokeza. Mwenyezi-Mungu hupangua mipango ya mataifa, na kuyatangua mawazo yao. Mpango wa Mwenyezi-Mungu hudumu milele; maazimio yake yadumu vizazi vyote. Heri taifa ambalo Mungu wake ni Mwenyezi-Mungu; heri wale aliowachagua kuwa watu wake mwenyewe!
Zaburi 33:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni BWANA kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe. Kwa kuwa neno la BWANA lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za BWANA. Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake. Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala. Nchi yote na imwogope BWANA, Wote wakaao duniani na wamche. Maana Yeye alisema, na ikawa; Na Yeye aliamuru, ikaumbika. BWANA huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huitangua mipango ya watu. Shauri la BWANA lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Zaburi 33:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni BWANA kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe. Kwa kuwa neno la BWANA lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za BWANA. Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake. Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala. Nchi yote na imwogope BWANA, Wote wakaao duniani na wamche. Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama. BWANA huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu. Shauri la BWANA lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Zaburi 33:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwimbieni BWANA kwa furaha, enyi wenye haki; kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Msifuni BWANA kwa kinubi, mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi. Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe. Maana neno la BWANA ni haki na kweli, ni mwaminifu kwa yote atendayo. BWANA hupenda uadilifu na haki; dunia imejaa upendo wake usiokoma. Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake. Ameyakusanya maji ya bahari kama kwenye chungu; vilindi vya bahari ameviweka katika ghala. Dunia yote na imwogope BWANA, watu wote wa dunia wamche. Kwa maana Mungu alisema, na ikawa, aliamuru na ikasimama imara. BWANA huzuia mipango ya mataifa, hupinga makusudi ya mataifa. Lakini mipango ya BWANA inasimama imara milele, makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.