Zaburi 35:1-10
Zaburi 35:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mwenyezi-Mungu, uwapinge hao wanaonipinga; uwashambulie hao wanaonishambulia. Utwae ngao yako na kingio lako, uinuke uje ukanisaidie! Chukua mkuki na sime yako dhidi ya wanaonifuatia. Niambie mimi kwamba utaniokoa. Waone haya na kuaibika, hao wanaoyanyemelea maisha yangu! Warudishwe nyuma kwa aibu, hao wanaozua mabaya dhidi yangu. Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, wakikimbizwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu! Njia yao iwe ya giza na utelezi, wakifukuzwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu! Maana walinitegea mitego bila sababu; walinichimbia shimo bila kisa chochote. Maangamizi yawapate wao kwa ghafla, wanaswe katika mtego wao wenyewe, watumbukie humo na kuangamia! Hapo mimi nitafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu; nitashangilia kwa kuwa yeye ameniokoa. Nitamwambia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote: “Wewe ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe! Wewe wawaokoa wanyonge makuchani mwa wenye nguvu, maskini na fukara mikononi mwa wanyanganyi.”
Zaburi 35:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, uwapinge hao wanaonipinga, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kikingio, Uinuke unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibike na kufedheheka, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafla, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia BWANA, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, BWANA, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini kutoka kwa mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.
Zaburi 35:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia BWANA, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, BWANA, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.
Zaburi 35:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee BWANA, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami. Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie. Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.” Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza warudishwe nyuma kwa hofu. Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa BWANA akiwafukuza. Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa BWANA akiwafuatilia. Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo, maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizo yao. Ndipo nafsi yangu itashangilia katika BWANA na kuufurahia wokovu wake. Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee BWANA? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”