Zaburi 37:27-40
Zaburi 37:27-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Achana na uovu, utende mema, nawe utaishi nchini daima; maana Mwenyezi-Mungu hupenda uadilifu, wala hawaachi waaminifu wake. Huwalinda hao milele; lakini wazawa wa waovu wataangamizwa. Waadilifu wataimiliki nchi, na wataishi humo milele. Mtu mwadilifu husema maneno ya hekima, kwa ulimi wake hunena yaliyo ya haki. Huizingatia moyoni mwake sheria ya Mungu wake; naye hatetereki katika mwenendo wake. Mtu mwovu humvizia mtu mwema na kujaribu kumuua; lakini Mwenyezi-Mungu hatamtia mtu mwema makuchani mwake, wala kumwacha apatilizwe akishtakiwa. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kushika njia yake, naye atakukuza uimiliki nchi, na kuwaona waovu wakiangamizwa. Nilimwona mwovu mdhalimu sana, alijiweka juu ya wote kama mierezi ya Lebanoni! Baadaye nikapita hapo, naye hakuwapo tena; nikamtafuta, lakini hakuonekana tena. Mwangalie mtu mwema, mtu mwadilifu; mtu anayependa amani hujaliwa wazawa. Lakini wakosefu wote wataangamizwa; na wazawa wao watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu, na kuwalinda wakati wa taabu. Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa; huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa, maana wanakimbilia usalama kwake.
Zaburi 37:27-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Jiepushe na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele. Kwa kuwa BWANA hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzawa wa wasio haki ataharibiwa. Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele. Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu. Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi. Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumwua. BWANA hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamwacha alaumiwe atakapohukumiwa. Wewe umngoje BWANA, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Utawaona Wasio haki wakiangamizwa. Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni. Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana. Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani. Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa. Na wokovu wa wenye haki una BWANA; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. Naye BWANA huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa kutoka kwa wasio haki na kuwaponya; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
Zaburi 37:27-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele. Kwa kuwa BWANA hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa. Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele. Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu. Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi. Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha. BWANA hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa. Wewe umngoje BWANA, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona. Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni. Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana. Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani. Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa. Na wokovu wa wenye haki una BWANA; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. Naye BWANA huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
Zaburi 37:27-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Acha ubaya na utende wema, nawe utaishi katika nchi milele. Kwa kuwa BWANA huwapenda wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake. Watalindwa milele, lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali. Wenye haki watairithi nchi, na kuishi humo milele. Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima, nao ulimi wake huzungumza lililo haki. Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake; nyayo zake hazitelezi. Watu waovu huvizia wenye haki, wakitafuta kuwaua; lakini BWANA hatawaacha mikononi mwao wala hatawaacha wahukumiwe kuwa wakosa wanaposhtakiwa. Mngojee BWANA, na uishike njia yake. Naye atakutukuza uirithi nchi, waovu watakapokatiliwa mbali, utaliona hilo. Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi kama mwerezi wa Lebanoni, lakini alitoweka mara na hakuonekana, ingawa nilimtafuta, hakupatikana. Watafakari watu wasio na hatia, wachunguze watu wakamilifu, kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani. Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa, mafanikio yao yatakatiliwa mbali. Wokovu wa wenye haki hutoka kwa BWANA, yeye ni ngome yao wakati wa shida. BWANA huwasaidia na kuwaokoa, huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi, kwa maana wanamkimbilia.