Zaburi 39:1-6
Zaburi 39:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilisema: “Nitayachunga maisha yangu, nisije nikatenda dhambi kwa usemi wangu. Nitafunga mdomo wangu waovu wawapo karibu nami.” Nilikuwa kama bubu, bila kusema kitu, nilinyamaza lakini sikupata nafuu. Mateso yangu yalizidi kuwa makali, mahangaiko yangu yakaniunguza moyoni. Kadiri nilivyowaza ndivyo nilivyotaabika, kisha maneno haya yakanitoka: “Ee Mwenyezi-Mungu, unijulishe mwisho wangu, siku zangu za kuishi zimenibakia ngapi, nijue yapitavyo kasi maisha yangu!” Kumbe umenipimia maisha mafupi sana! Maisha yangu si kitu mbele yako. Hakika, kila binadamu ni kama pumzi tu! Kweli, kila mtu anapita kama kivuli; jitihada zake zote ni bure tu; anakusanya mali, asijue atakayeipata!
Zaburi 39:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nilisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya awapo mbele yangu. Nilikuwa sisemi, nilinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi. Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nilisema kwa ulimi wangu, BWANA, unijulishe mwisho wangu, Na idadi ya siku zangu ni ngapi; Nijue jinsi maisha yangu yalivyo mafupi. Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili. Kweli, watu wote hupita kama kivuli; Wao hujisumbua bure tu; Wanajirundikia mali wala hawajui ni nani atakayeirithi.
Zaburi 39:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nalisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu. Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi. Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nalisema kwa ulimi wangu, BWANA, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu. Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili. Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.
Zaburi 39:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi; nitaweka lijamu kinywani mwangu wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.” Lakini niliponyamaza kimya na kutulia, hata pasipo kusema lolote jema, uchungu wangu uliongezeka. Moyo wangu ulipata moto ndani yangu, nilipotafakari, moto uliwaka, ndipo nikasema kwa ulimi wangu: “Ee BWANA, nijulishe mwisho wa maisha yangu na hesabu ya siku zangu; nijalie kujua jinsi maisha yangu yanavyopita upesi. Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi; muda wangu wa kuishi ni kama hauna thamani kwako. Maisha ya kila mwanadamu ni kama pumzi. Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayeifaidi.