Zaburi 45:1-8
Zaburi 45:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Moyo wangu umejaa mawazo mema: Namtungia mfalme shairi langu, ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi. Wewe u mzuri kuliko wanadamu wote, maneno yako ni fadhili tupu. Kwa hiyo Mungu amekubariki milele. Jifunge upanga wako, ewe shujaa! Wewe ni mtukufu na mwenye fahari. Songa mbele kwa utukufu upate ushindi, utetee ukweli na kulinda haki. Mkono wako utende mambo makuu. Mishale yako ni mikali, hupenya mioyo ya maadui za mfalme; nayo mataifa huanguka chini yako. Kiti chako cha enzi ni imara, chadumu milele kama cha Mungu. Wewe watawala watu wako kwa haki. Wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua, na kukupa furaha kuliko wenzako. Mavazi yako yanukia marashi na udi, wanamuziki wakuimbia katika majumba ya pembe za ndovu.
Zaburi 45:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Moyo wangu umefurika kwa jambo jema, Mimi nasema niliyomfanyia mfalme; Ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi. Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele. Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako. Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli, upole na haki Na mkono wako wa kulia Utakutendea mambo ya ajabu. Mishale yako ni mikali, katika mioyo ya adui za mfalme; Watu huanguka chini yako. Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako. Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.
Zaburi 45:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi. Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele. Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako. Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha. Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme. Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako. Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.
Zaburi 45:1-8 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema ninapomsimulia mfalme mabeti yangu; ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi. Wewe ni bora kuliko watu wengine wote na midomo yako imepakwa neema, kwa kuwa Mungu amekubariki milele. Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu, jivike fahari na utukufu. Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi, kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki, mkono wako wa kuume na uoneshe matendo ya kutisha. Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme, mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako. Ee Mungu, kiti chako cha enzi kitadumu milele na milele, fimbo ya utawala wa haki itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako. Unaipenda haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako, kwa kukupaka mafuta ya furaha. Mavazi yako yote yana harufu nzuri ya manemane, udi na mdalasini; kutoka majumba ya kifalme yaliyopambwa kwa pembe za ndovu, sauti za vinanda vya nyuzi zinakufanya ufurahi.