Zaburi 46:1-11
Zaburi 46:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema. Mataifa yalighadhibika, falme zikataharuki; Alitoa sauti yake, nchi ikayeyuka. BWANA wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. Njoni myatazame matendo ya BWANA, Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari. Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu, Nitakuzwa katika mataifa, nitakuzwa katika nchi. BWANA wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Zaburi 46:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini; hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake. Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu, makao matakatifu ya Mungu Mkuu. Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa; Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema. Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika; Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka. Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu; oneni maajabu aliyoyafanya duniani. Hukomesha vita popote duniani, huvunjavunja pinde na mikuki, nazo ngao huziteketeza. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
Zaburi 46:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye Juu. Mungu yu katikati ya mji hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema. Mataifa yanaghadhibika na falme kutetemeka; Anatoa sauti yake, nchi inayeyuka. BWANA wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. Njoni muyatazame matendo ya BWANA, Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari. Tulieni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu, Nitakuzwa katika mataifa, nitakuzwa katika nchi. BWANA wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
Zaburi 46:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari. Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka, milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake. Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu, mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi. Mungu yuko katikati yake, hautaanguka, Mungu atausaidia asubuhi na mapema. Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka, Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka. BWANA Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. Njooni mkaone kazi za BWANA jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. Anakomesha vita hata miisho ya dunia, anakata upinde na kuvunjavunja mkuki, anateketeza ngao kwa moto. “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu; nitatukuzwa katikati ya mataifa, nitatukuzwa katika dunia.” BWANA Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi; Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.