Zaburi 47:1-9
Zaburi 47:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe. Kwa kuwa BWANA Aliye Juu, mwenye kuogofya, Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. Amewatiisha watu wa nchi chini yetu, Na mataifa chini ya miguu yetu. Ametuchagulia urithi wetu, Fahari ya Yakobo ampendaye. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, BWANA kwa sauti ya baragumu. Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa; Imbeni sifa kwa mfalme wetu, imbeni sifa. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa zaburi. Mungu ayatawala mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. Wakuu wa watu wamekusanyika, Kama watu wa Mungu wa Abrahamu. Maana ngao za dunia zina Mungu, Ametukuka sana.
Zaburi 47:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Enyi watu wote, pigeni makofi! Msifuni Mungu kwa sauti za shangwe! Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, anatisha. Yeye ni Mfalme mkuu wa ulimwengu wote. Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa, ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu. Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu, ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda. Mungu amepanda juu na vigelegele, Mwenyezi-Mungu na sauti ya tarumbeta. Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni! Mwimbieni mfalme wetu sifa, mwimbieni! Mwimbieni Mungu sifa kwa tenzi; maana yeye ni mfalme wa ulimwengu wote. Mungu anayatawala mataifa yote; amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu. Viongozi wa watu wa mataifa wanakusanyika, wanajiunga na watu wa Mungu wa Abrahamu, maana nguvu zote duniani ni zake Mungu, yeye ametukuka sana.
Zaburi 47:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe. Kwa kuwa BWANA Aliye juu, mwenye kuogofya, Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. Atawatiisha watu wa nchi chini yetu, Na mataifa chini ya miguu yetu. Atatuchagulia urithi wetu, Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, BWANA kwa sauti ya baragumu. Mwimbieni Mungu, naam, imbeni; Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili. Mungu awamiliki mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. Wakuu wa watu wamekusanyika, Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu. Maana ngao za dunia zina Mungu, Ametukuka sana.
Zaburi 47:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Pigeni makofi, enyi mataifa yote, mpigieni Mungu kelele za shangwe! Jinsi gani alivyo wa kutisha, BWANA Aliye Juu Sana, Mfalme mkuu juu ya dunia yote! Ametiisha mataifa chini yetu watu wengi chini ya miguu yetu. Alituchagulia urithi wetu, fahari ya Yakobo, aliyempenda. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, BWANA kwa sauti za tarumbeta. Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa, mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa. Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote, mwimbieni zaburi za sifa. Mungu anatawala juu ya mataifa, Mungu ameketi juu ya kiti chake cha enzi kitakatifu. Wakuu wa mataifa wanakusanyika kama watu wa Mungu wa Abrahamu, kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu; yeye ametukuka sana.